Zubeidah Kananu

Image of Zubeidah Kananu

Zubeidah alijiunga na kampuni ya Standard Januari Mwaka 2007. Alipitia mafunzo kwa muda wa miezi mitatu kisha akafanya kazi kwa kandarasi kwa muda wa mwaka mmoja.

Mwaka 2009 aliajiriwa kama mfanyakazi wa kudumu na kuwa ripota wa KTN. Alipandishwa daraja miezi michache baadaye na kuwa ripota mkuu. Mwaka 2012 alipandishwa daraja tena na kuwa mhariri wa masuala ya kisiasa katika meza ya KTN LEO. Yeye pia ni mtayarishi wa taarifa za KTN LEO mbali na kuwa msomaji habari wa taarifa kwa lugha ya Kiswahili.

Zubeidah amefanya mahojiano na viongozi mbalimbali hasa wanasiasa na pia watu mashuhuri kitaifa na kimataifa. Miongoni mwa viongozi barani aliowahoji ni Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, Rais wa Kwanza wa Zambia Kenneth Kaunda, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, aliyekuwa naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka miongoni mwa wengine.

Baadhi ya hafla kuu alizozishughulikia katika kuandaa ripoti na mahojiano ni Uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, Kampeni na Kura ya maoni ya Katiba mwaka 2009, Uzinduzi wa Katiba Mpya Mwaka 2010, Kongamano lililoongozwa na Kofi Annan la kudadisi maridhiano nchini lililopeperushwa na KTN kwa ushirikiano na runinga ya Kitaifa ya Afrika Kusini SABC, Kampeni na Uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, Kuapishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuchaguliwa, Kesi za machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/08 zinazoendelea nchini Uholanzi-ICC, na Kongamano la Wabunge wa Mataifa ya bara Afrika nchini Afrika Kusini.

Zubeidah amevitayarisha pia vipindi mbali mbali vya kisiasa ambavyo vimekuwa na mvuto mkubwa mfano makala kumhusu Rais mstaafu Daniel Arap Moi (90 ya SULUBU), Historia ya Siasa ya chama cha ODM, na Historia ya Siasa ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga (Kiwambo Cha Agwambo). Vile vile ni mtayarishi wa “BUNGE LAKO” Makala Maalum ya Kisiasa yanayoangazia maisha ya wanasiasa na athari za siasa kwa Mwananchi. Mbali na Runinga pia nimekuwa msomaji wa taarifa katika kituo cha Redio Maisha.

Alizaliwa na kusomea katika Kaunti ya Meru kabla ya kujiunga na taasisi mbali mbali kama vile Kenya School of Professional Studies, Shang’ Tao Media, Crossworld Institute na kuhitimu katika somo la uanahabari. Kisha nilijiunga na chuo kikuu cha Africa Nazarene jijini Nairobi kwa shahada katika somo la Peace and Conflict Resolution Studies.